Wachunguzi wa masuala ya mazingira
nchini Urusi wanajaribu kubaini sababu iliyoyafanya maji ya mto ulio
karibu na kiwanda cha nikeli cha kampuni ya Norilsk Nickel kubadilika na
kuwa ya rangi nyekundu.
Picha za maji ya mto Daldykan ambayo yamebadilika rangi zimesambazwa sana katika vyombo vya habari Urusi.
Gazeti
la serikali la Rossiiskaya Gazeta linasema kuvuja kwa bomba la
kusafirisha taka za mchanganyiko wa shaba nyekundu na nikeli huenda
likawa kiini cha maji hayo kubadilika rangi.
Norilsk Nickel ndiyo mzalishaji mkubwa zaidi wa nikeli na palladium duniani.
Kampuni hiyo ina vinu na tanuri nyingi rasi ya Taimyr eneo la
Krasnoyarsk katika jimbo la Siberia. Ujenzi wa vinu hivyo vikubwa
ulifanyika enzi za muungano wa Usovieti.
Kampuni hiyo ina kiwanda
kwa jina Nadezhda karibu na mto Daldykan lakini maafisa wake wanasema
hawajapata dalili zozote za uchafuzi kutoka kwa kiwanda hicho.
Rais wa kampuni hiyo ni bilionea Vladimir Potanin.