Hospitali hiyo imesema inatarajia kuanza kuwapeleka wataalamu nje ya nchi kuanzia Septemba, mwaka huu kwa ajili ya kusoma kwa muda wa miezi miwili hadi minne ili Januari huduma hiyo ianze kutolewa.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Profesa Lawrence Mseru wakati akiwatunuku vyeti wafanyakazi bora 53, ambapo alisema, kuanzishwa kwa huduma hiyo kutapunguza watoto waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi.
“…jambo hili tunatarajia kupunguza na kuondoa kitendo cha kuwasafirisha wagonjwa nje ya nchi kwani tunatarajia kutoa huduma ya kupandikiza vifaa vya kusikia kwa watoto wadogo, pia tutaanza kupandikiza figo,” alisema Profesa Mseru.
Alisema mbali na kutoa huduma hiyo hospitali hiyo inatoa huduma ya kusafisha figo, magonjwa ya tumbo, kufanya upasuaji mbalimbali huku akibainisha hospitali hiyo inahitaji ukarabati kutokana na miundombinu yake kuchakaa.
Profesa Mseru alisema, kutokana na ukubwa wa hospitali hiyo wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya wagonjwa, huku miundombinu yake ikiwa na changamoto nyingi hasa katika kipindi cha mvua, upatikanaji wa vifaa vya kufulia nguo za wagonjwa, kuteketeza taka ngumu na vifaa vingine.
“Aidha, tuna upungufu wa rasilimali fedha katika utoaji huduma au kuwapa motisha wafanyakazi wetu,” alisema.
Alisema kila mwezi hospitali hiyo inalazimika kulilipa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) Sh milioni 200 hadi 220 huku Shirika la Dawasco wakililipa Sh milioni 100 kwa mwezi.
Akizungumzia ulipaji wa majengo, Prof Mseru alisema Manispaa inawadai Sh milioni 20 kwa mwezi.Katika kipindi cha miezi 6 iliyopita wastani wa pato la hospitali kwa mwezi ilikuwa sh bilioni 2.3 hadi sh bilioni 2.5; huku mahitaji kwa mwezi ya kawaida ikiwa sh bilioni 4.
Mbali na hilo, Prof Mseru alisema wanatarajia kukarabati vyumba vya upasuaji na kuongeza kutoka idadi ya vyumba 13 hadi kufikia vyumba 19 na kuhakikisha vyumba vinakuwa vikubwa, sanjari na kuongeza vitanda katika chumba cha wagonjwa wenye uhitaji wa uangalizi(ICU), kutoka vitanda 21 hadi kufikia vitanda 60.
Post a Comment