Halloween party ideas 2015

Makamo wa Rais, Samia Suluhu Hassan akifungua mkutano wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbli (MUHAS) jijini Dar es Salaam..
HISTORIA ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam imeanza tangu mwaka 1963, chuo kikiwa ndani ya hospitali iliyoitwa Princess Margaret kikiwa na wanafunzi 10 wanaochukua mchepuo wa udaktari au upasuaji pekee.
Kwa muda mrefu, Muhas imekuwa chuo cha elimu ya afya kama sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Mwaka 2007 Muhas ilipandishwa hadhi na kuwa chuo kikuu kinachojitegemea chenye idara nne ambazo ni utaalamu wa meno, uganga, uuguzi na dawa.
Kwa sasa, Muhas ina takribani wanafunzi 4,000 wa nchini na kimataifa wanaochukua michepuo mbalimbali ambayo ni madaktari, wauguzi, mafamasia, waganga wa meno, mabwana afya, mabwana mazingira na elimu ya juu ya afya. Chuo hicho kiko kwenye mchakato wa upanuzi kupitia mradi wa ujenzi wa kampasi ya Mlonganzila.
Ikikamilika, inatarajiwa kudahili wanafunzi zaidi ya 15,000 na itaongeza michepuo au kozi. Muhas imekuwa ni hazina kuu kwa serikali kutokana na kuwa chanzo cha kuzalisha wataalamu wa afya na madaktari bingwa.
Vile vile ni miongoni mwa maeneo yanayotoa mchango mkubwa wa utafiti wa masuala yanayogusa eneo la afya. Miongoni mwa utafiti unaogusa sekta ya afya uliofanywa na chuo hicho na kuleta mabadiliko katika jamii, ni uliobaini njia ya kisasa na rahisi ya kupima virusi vya Ukimwi na malaria ambayo mgonjwa huchukua dakika mchache kupata majibu ya vipimo vyake.
“Sisi ndiyo tuliogundua njia mbadala bora na rahisi kwa mgonjwa ya kupima malaria kwa kutumia vifaa vya kisasa ambayo pia sasa inapimia virusi vya Ukimwi na mgonjwa kupatiwa majibu yake kwa muda mfupi kuliko mwanzo,” anasema Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Ephata Kaaya.
Katika mkakati wake wa kuboresha zaidi utafiti nchini, hivi karibuni chuo hicho kilifanya mkutano wa nne wa utafiti wa kisayansi. Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Kaaya, mikutano ya utafiti inalenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili sekta ya afya na hatimaye kupunguza umasikini.
Katika mkutano huo ulioongozwa na kauli mbiu inayohamasisha uwekezaji katika utafiti wa afya na mafunzo kwa maendeleo endelevu, Kaaya anasema Muhas imejipanga kuhakikisha inaboresha zaidi tafiti zake kwa kuongeza maeneo mengi ya kufanyia. Anasema kipaumbele kikubwa ni kwenye utafiti wa magonjwa ya malaria, kifua kikuu, Ukimwi, afya ya mtoto, majeraha na elimu ya afya kwa ujumla.
“Tunatambua umuhimu wa sisi kama watalaamu kuendelea kuimarisha zaidi eneo hili la utafiti. Lengo letu hasa ni kuhakikisha vijana wengi zaidi wanajihusisha na kushiriki katika tafiti zetu mbalimbali ili kujenga taifa lenye vijana wenye ujuzi katika masuala ya utafiti wa kisayansi,” anasisitiza Profesa Kaaya.
Anasema tangu chuo hicho kianzishwe miaka 50 iliyopita, kimefanya utafiti mbalimbali ambao umesaidia kuwezesha wizara kutunga sera zinazoendana na hali halisi. Anatoa mfano wa Sera ya Ukimwi na Malaria kuwa ni matokeo ya tafiti zao.
Aidha, Profesa Kaaya anasema Muhas katika mpango wake wa kuimarisha eneo la utafiti, imekuwa ikitoa mafunzo ya utafiti kwa wataalamu wake. Asilimia 95 ya wataalamu hao inatajwa kuwa wameshanufaika na mafunzo hayo kupitia mfuko wa mafunzo.
“Ukweli ni kwamba Muhas tumejitahidi sana kuimarisha eneo hili la utafiti kupitia mikutano hii ya mafunzo na utafiti na tumejiwekea lengo kuwa kiungo cha kuongeza ujuzi kwa wanafunzi wa ndani na nje,” anasema.
Mkuu huyo wa chuo anaeleza zaidi mpango wa chuo hicho wa kushirikisha vijana zaidi katika masuala ya utafiti. Anasema kwenye mikutano yake, chuo kimekuwa kikishirikisha wanafunzi kuwasilisha mada kuhusu tafiti mbalimbali na kila mwaka, ushiriki wa wanafunzi hao huongezeka.
Mathalani, mkutano wao wa mwaka huu uliokuwa na jumla ya mada 170 za kuwasilishwa, kati ya hizo, mada 70 ambazo ni sawa na asilimia 30 ziliwasilishwa na wanafunzi. Pamoja na mafanikio yote, Profesa Kaaya anasema sekta ya utafiti imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali , kubwa zaidi ikiwa ni uhaba wa fedha.
“Taifa hili bado linakabiliwa na matatizo ya afya na bila sayansi huwezi kuelewa mbinu za kutatua matatizo yanayotukabili, hivyo tutaendelea kufanya utafiti kutatuta changamoto zinazoikabili jamii yetu,” anasema.
Hata hivyo, changamoto ya fedha inaonekana kupatiwa ufumbuzi kutokana na serikali itahakikisha inaongeza bajeti ya sekta ya afya. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alifungua mkutano wa nne, anasema serikali imejipanga kuongeza bajeti ya sekta ya afya hadi kufikia asilimia 15 kama ambavyo nchi imeridhia katika Azimio la Abuja mwaka 2001.
Hatua hiyo ya kuongeza fedha za bajeti kwa sekta ya afya inatajwa kuwa itawezesha Tanzania pamoja na nchi nyingine zinazoendelea kuboresha eneo la utafiti litakaloweza kuibua masuala nyeti yagusayo jamii moja kwa moja.

Makamu wa Rais anasema kwa kuanzia, katika bajeti ya mwaka 2016/17 serikali imeongeza fedha kwenye sekta ya utafiti. Hata hivyo anasema kiwango hakijafikia asilimia 15 kama ilivyoridhiwa.
“Nichukue fursa hii kuwahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa sekta ya afya lakini pia inatambua mchango mkubwa wa utafiti unaofanywa na wataalamu wa afya. Nawahakikishia katika bajeti zetu zijazo, serikali itahakikisha asilimia hii 15 inafikiwa,” anasisitiza.
Kulingana na bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, Sh bilioni 845 ndizo zilizopitishwa. Kiasi hicho kiko chini ya asilimia 10 ya bajeti nzima ambayo ni Sh trilioni 29. Samia anawataka wataalamu wa masuala ya afya pia kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili katika utekelezaji wa miradi muhimu ikiwemo utafiti.
Anasisitiza kuwa misaada mingi huwa na muda wa kukatishwa hali ambayo inaweza kusababisha malengo ya mradi husika yasifikiwe. Anashauri uongozi wa chuo kujenga uhusiano wa karibu na viwanda vya ndani na kimataifa kwa ajili ya kuimarisha eneo la utafiti na mafunzo.
Ushauri zaidi unaotolewa ni ushirikishaji wa vijana wengi kwenye eneo la utafiti wa kisayansi kwa maendeleo ya taifa. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasisitiza juu ya hilo akitaka vijana wengi wengi washirikishwe katika utafiti ili kujenga taifa lenye vijana watafiti na wataalamu wa kutosha.
Ummy ambaye aliwakilishwa na Katibu Mkuu wa wizara yake, John Michael; kufunga mkutano huo wa nne wa utafiti wa kisayansi, anasema utafiti wa kisayansi ni muhimu kwa nchi yoyote. Umuhimu wake unatajwa kuwa ni kuhakikisha nchi inafikia malengo yake ya maendeleo, ikiwemo utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
Waziri Ummy anataja utafiti huo wa kisayansi kuwa ni kiungo muhimu kinachowezesha nchi kufikia malengo hayo ya umoja wa mataifa kwa kuwa ndiyo unaotoa mwongozo wa kisayansi na mipango juu ya namna ya kuyafikia. Anasema ni lazima taifa lianze kuchukua hatua sasa na kuhakikisha mfumo wa kitaifa wa huduma za afya, uchumi unakabili mzigo wa magonjwa kwa njia ya utafiti.


Post a Comment

Powered by Blogger.