Makamo wa Rais, Samia Suluhu Hassan
akifungua mkutano wa kisayansi ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbli (MUHAS) jijini Dar es Salaam..
HISTORIA ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili (MUHAS) jijini Dar es Salaam imeanza tangu mwaka 1963,
chuo kikiwa ndani ya hospitali iliyoitwa Princess Margaret kikiwa na wanafunzi
10 wanaochukua mchepuo wa udaktari au upasuaji pekee.
Kwa muda mrefu, Muhas imekuwa chuo
cha elimu ya afya kama sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Mwaka
2007 Muhas ilipandishwa hadhi na kuwa chuo kikuu kinachojitegemea chenye idara
nne ambazo ni utaalamu wa meno, uganga, uuguzi na dawa.
Kwa sasa, Muhas ina takribani
wanafunzi 4,000 wa nchini na kimataifa wanaochukua michepuo mbalimbali ambayo
ni madaktari, wauguzi, mafamasia, waganga wa meno, mabwana afya, mabwana
mazingira na elimu ya juu ya afya. Chuo hicho kiko kwenye mchakato wa upanuzi
kupitia mradi wa ujenzi wa kampasi ya Mlonganzila.
Ikikamilika, inatarajiwa kudahili
wanafunzi zaidi ya 15,000 na itaongeza michepuo au kozi. Muhas imekuwa ni
hazina kuu kwa serikali kutokana na kuwa chanzo cha kuzalisha wataalamu wa afya
na madaktari bingwa.
Vile vile ni miongoni mwa maeneo
yanayotoa mchango mkubwa wa utafiti wa masuala yanayogusa eneo la afya.
Miongoni mwa utafiti unaogusa sekta ya afya uliofanywa na chuo hicho na kuleta
mabadiliko katika jamii, ni uliobaini njia ya kisasa na rahisi ya kupima virusi
vya Ukimwi na malaria ambayo mgonjwa huchukua dakika mchache kupata majibu ya
vipimo vyake.
“Sisi ndiyo tuliogundua njia mbadala
bora na rahisi kwa mgonjwa ya kupima malaria kwa kutumia vifaa vya kisasa
ambayo pia sasa inapimia virusi vya Ukimwi na mgonjwa kupatiwa majibu yake kwa
muda mfupi kuliko mwanzo,” anasema Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Ephata Kaaya.
Katika mkakati wake wa kuboresha
zaidi utafiti nchini, hivi karibuni chuo hicho kilifanya mkutano wa nne wa
utafiti wa kisayansi. Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Kaaya, mikutano
ya utafiti inalenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokabili sekta ya afya
na hatimaye kupunguza umasikini.
Katika mkutano huo ulioongozwa na
kauli mbiu inayohamasisha uwekezaji katika utafiti wa afya na mafunzo kwa
maendeleo endelevu, Kaaya anasema Muhas imejipanga kuhakikisha inaboresha zaidi
tafiti zake kwa kuongeza maeneo mengi ya kufanyia. Anasema kipaumbele kikubwa
ni kwenye utafiti wa magonjwa ya malaria, kifua kikuu, Ukimwi, afya ya mtoto,
majeraha na elimu ya afya kwa ujumla.
“Tunatambua umuhimu wa sisi kama
watalaamu kuendelea kuimarisha zaidi eneo hili la utafiti. Lengo letu hasa ni
kuhakikisha vijana wengi zaidi wanajihusisha na kushiriki katika tafiti zetu
mbalimbali ili kujenga taifa lenye vijana wenye ujuzi katika masuala ya utafiti
wa kisayansi,” anasisitiza Profesa Kaaya.
Anasema tangu chuo hicho kianzishwe
miaka 50 iliyopita, kimefanya utafiti mbalimbali ambao umesaidia kuwezesha
wizara kutunga sera zinazoendana na hali halisi. Anatoa mfano wa Sera ya Ukimwi
na Malaria kuwa ni matokeo ya tafiti zao.
Aidha, Profesa Kaaya anasema Muhas
katika mpango wake wa kuimarisha eneo la utafiti, imekuwa ikitoa mafunzo ya
utafiti kwa wataalamu wake. Asilimia 95 ya wataalamu hao inatajwa kuwa
wameshanufaika na mafunzo hayo kupitia mfuko wa mafunzo.
“Ukweli ni kwamba Muhas tumejitahidi
sana kuimarisha eneo hili la utafiti kupitia mikutano hii ya mafunzo na utafiti
na tumejiwekea lengo kuwa kiungo cha kuongeza ujuzi kwa wanafunzi wa ndani na
nje,” anasema.
Mkuu huyo wa chuo anaeleza zaidi
mpango wa chuo hicho wa kushirikisha vijana zaidi katika masuala ya utafiti.
Anasema kwenye mikutano yake, chuo kimekuwa kikishirikisha wanafunzi
kuwasilisha mada kuhusu tafiti mbalimbali na kila mwaka, ushiriki wa wanafunzi
hao huongezeka.
Mathalani, mkutano wao wa mwaka huu
uliokuwa na jumla ya mada 170 za kuwasilishwa, kati ya hizo, mada 70 ambazo ni
sawa na asilimia 30 ziliwasilishwa na wanafunzi. Pamoja na mafanikio yote,
Profesa Kaaya anasema sekta ya utafiti imekuwa ikikabiliwa na changamoto
mbalimbali , kubwa zaidi ikiwa ni uhaba wa fedha.
“Taifa hili bado linakabiliwa na
matatizo ya afya na bila sayansi huwezi kuelewa mbinu za kutatua matatizo
yanayotukabili, hivyo tutaendelea kufanya utafiti kutatuta changamoto
zinazoikabili jamii yetu,” anasema.
Hata hivyo, changamoto ya fedha
inaonekana kupatiwa ufumbuzi kutokana na serikali itahakikisha inaongeza bajeti
ya sekta ya afya. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alifungua mkutano
wa nne, anasema serikali imejipanga kuongeza bajeti ya sekta ya afya hadi kufikia
asilimia 15 kama ambavyo nchi imeridhia katika Azimio la Abuja mwaka 2001.
Hatua hiyo ya kuongeza fedha za
bajeti kwa sekta ya afya inatajwa kuwa itawezesha Tanzania pamoja na nchi
nyingine zinazoendelea kuboresha eneo la utafiti litakaloweza kuibua masuala
nyeti yagusayo jamii moja kwa moja.
Makamu wa Rais anasema kwa kuanzia,
katika bajeti ya mwaka 2016/17 serikali imeongeza fedha kwenye sekta ya
utafiti. Hata hivyo anasema kiwango hakijafikia asilimia 15 kama ilivyoridhiwa.
“Nichukue fursa hii kuwahakikishia
kuwa Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa sekta ya afya lakini pia
inatambua mchango mkubwa wa utafiti unaofanywa na wataalamu wa afya.
Nawahakikishia katika bajeti zetu zijazo, serikali itahakikisha asilimia hii 15
inafikiwa,” anasisitiza.
Kulingana na bajeti ya Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyowasilishwa bungeni hivi
karibuni, Sh bilioni 845 ndizo zilizopitishwa. Kiasi hicho kiko chini ya
asilimia 10 ya bajeti nzima ambayo ni Sh trilioni 29. Samia anawataka wataalamu
wa masuala ya afya pia kuondokana na utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili
katika utekelezaji wa miradi muhimu ikiwemo utafiti.
Anasisitiza kuwa misaada mingi huwa
na muda wa kukatishwa hali ambayo inaweza kusababisha malengo ya mradi husika
yasifikiwe. Anashauri uongozi wa chuo kujenga uhusiano wa karibu na viwanda vya
ndani na kimataifa kwa ajili ya kuimarisha eneo la utafiti na mafunzo.
Ushauri zaidi unaotolewa ni
ushirikishaji wa vijana wengi kwenye eneo la utafiti wa kisayansi kwa maendeleo
ya taifa. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu anasisitiza juu ya hilo akitaka vijana wengi wengi washirikishwe katika
utafiti ili kujenga taifa lenye vijana watafiti na wataalamu wa kutosha.
Ummy ambaye aliwakilishwa na Katibu
Mkuu wa wizara yake, John Michael; kufunga mkutano huo wa nne wa utafiti wa
kisayansi, anasema utafiti wa kisayansi ni muhimu kwa nchi yoyote. Umuhimu wake
unatajwa kuwa ni kuhakikisha nchi inafikia malengo yake ya maendeleo, ikiwemo
utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).
Waziri Ummy anataja utafiti huo wa
kisayansi kuwa ni kiungo muhimu kinachowezesha nchi kufikia malengo hayo ya
umoja wa mataifa kwa kuwa ndiyo unaotoa mwongozo wa kisayansi na mipango juu ya
namna ya kuyafikia. Anasema ni lazima taifa lianze kuchukua hatua sasa na
kuhakikisha mfumo wa kitaifa wa huduma za afya, uchumi unakabili mzigo wa
magonjwa kwa njia ya utafiti.