WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu ameziagiza hospitali zote za rufaa nchini ngazi ya Mikoa, Kanda
na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wa
fistula.
Aliyasema hayo mjini Tanga kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo
katika uzinduzi wa kambi ya matibabu ya wagonjwa wa fistula itakayodumu
kwa kipindi cha wiki moja kuanzia juzi hadi Agosti 19, mwaka huu.
Alisema tatizo la fistula limekuwa likiongezeka kila siku na
waathirika wengi ni akinamama wa vijijini na wale wa kipato cha chini
ambao wanashindwa kupata huduma sahihi za afya ikiwemo kuchelewa kwenda
kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakati wa kujifungua.
Takribani akinamama 2,500 hadi 3,000 hupata tatizo la ugonjwa wa
fistula kila mwaka japo idadi hii ni ndogo sana kuliko hali halisi
ilivyo kwa kuwa wagonjwa wengi hunyanyapaliwa na familia zao na jamii
kwa ujumla.
“Serikali ya Awamu ya Tano imejikita zaidi katika kuwahudumia
wanyonge, kwa mamlaka niliyopewa natoa msamaha wa kulipia matibabu ya
fistula ili kuwapunguzia mateso wanawake hawa. Kwa kuwa wenye tatizo la
fistula ni wanawake wa kipato cha chini na wa vijijini, naziagiza
hospitali zote za rufaa za mikoa na kanda kutoa matibabu ya fistula bure
kwa wagonjwa watakaofika kutaka huduma hiyo,” alisema Ummy.
Alisema ili kuhakikisha huduma hiyo inatolewa, ameziagiza hospitali
hizo kuandaa kambi za matibabu ya fistula angalau mara moja kila mwaka
na apatiwe taarifa.
Aidha, ameeleza kuwa akinamama wengi wenye tatizo la fistula wamekuwa
wakishindwa kufanya shughuli za uchumi kama biashara ndogo ndogo kwa
kuwa ugonjwa huu ni wa aibu ambao husababisha watu kunyanyapaliwa na
jamii.
Pia alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika
kukabiliana na tatizo la ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa
miundombinu kwa ajili ya huduma za ujauzito na uzazi, mafunzo ya huduma
za dharura za uzazi kwa watoa huduma za afya pamoja na usimamizi
shirikishi, uimarishaji wa ubora wa huduma za ujauzito na uzazi,
kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya ujauzito na
uzazi, kuimarisha mifumo ya rufaa na kuhakikisha huduma za dharura za
uzazi zinapatikana hasa maeneo ya vijijini na wataalamu waliobobea
katika maeneo hayo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Asha Mahita alisema Hospitali ya
Bombo ina changamoto ya kuwa na miundombinu chakavu, uhaba wa vifaa tiba
na watumishi kiasi ambacho wanashindwa kutoa huduma ya kutibu akinamama
wenye tatizo la fistula kwa kuwa hawana wataalamu waliobobea katika
maeneo hayo.
Post a Comment